Ruto, viongozi wa Afrika wahudhuria uapisho wa Rais Mahama wa Ghana

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais mpya wa Ghana John Mahama akiwa na Rais William Ruto wakati wa hafla ya kuapishwa mjini Accra

Rais William Ruto alikuwa miongoni mwa viongozi kadhaa wa bara la Afrika waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Ghana John Dramani Mahama. 

Hafla hiyo ya leo Jumanne ilifanyika katika uwanja maarufu wa Black Star katika mji mkuu wa nchi hiyo, Accra.

Akizungumza baada ya kula kiapo, Rais Mahama aliziahidi kampuni na wawekezaji kuwa milango ya biashara ya Ghana iko wazi, akiahidi mfumo ulio wazi na wa haki zaidi wa utozaji kodi ili kuhuisha uchumi wa nchi hiyo.

Aidha, Rais Mahama alisema atakutana na viongozi wa biashara ili kusisitiza kuwa nchi yake iko wazi kwa biashara kando na kuainisha mipango ya uchumi wa saa 24.

Alipokuwa nchini Kenya mwezi jana, Mahama alikutana na Rais Ruto na wawili hao kukubaliana kuwa nchi hizo mbili zitaimarisha ushirikiano wao katika biashara na uwekezaji, kilimo, madini, utalii na gesi.

Pia waliahidi kupanua fursa kwa ajili ya raia wa nchi hizo mbili na kuwawezesha kusafiri na kufanya biashara.

Mapema leo Jumanne, Ruto alikutana na Marais Faure Gnassingbé wa Togo na Gideon Boko wa Botswana na pia Makamu Rais wa Equatorial Guinea Teodoro Nguema Obiang Mangue jijini Accra.

Wakati wa mkutano wao, wote hao waliahidi kuunga mkono azima ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.

Uchaguzi wa kuwania wadhifa huo utaandaliwa mwezi ujao.

Raila atakabiliana na wagombea wengine wawili kutoka Djibouti na Madagascar katika kuwania wadhifa huo ambao kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki anayeondoka.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *