Ruto: Uzalishaji maziwa kuongezwa maradufu nchini

Martin Mwanje
2 Min Read

Uzalishaji wa maziwa humu nchini utaongezwa maradufu katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuwapanulia wakulima fursa.  

Rais William Ruto amesema serikali imeweka mpango kabambe ambao utasababisha kuongezeka kwa uzalishaji kutoka lita bilioni 5.2 hadi bilioni 10 kwa mwaka.

Alisema maziwa ni moja ya sekta zinazoiletea nchi hii mapato ya juu, ikileta zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.

Alielezea kuwa serikali itaweka mitambo ya kisasa kwenye kampuni ya Kenya Cooperative Creameries, KCC na kuweka vipozea maziwa kote nchini ili maziwa yaweze kuchakatwa.

“Tunataka kupata fedha zaidi kutoka kwenye maziwa yalioongezewa thamani. Wakulima wetu hawanufaiki kwa sababu wamekuwa wakiuza maziwa ambayo hayajachakatwa,” alisema Rais Ruto.

Alisema nchi hii ina vituo vya kutosha vya kutengeneza poda na maziwa ya kukaa muda mrefu ili kuhakikisha maziwa ya ziada hayaharibiki.

“Pia tutaepukana na matapeli ili wakulima wapate mapato ya juu kutoka kwenye maziwa yao.”

Ruto aliyasema hayo leo Jumanne katika eneo la Kiganjo, kaunti ya Nyeri, alikozindua mtambo wa kisasa wa kuchakata maziwa wa kampuni ya KCC ya Kiganjo.

Mtambo huo umewekwa mabomba mapya ya kuchakata maziwa ya ngamia na maji ya kunywa.

Naibu Rais Rigathi Gachagua na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ni miongoni mwa waliokuwapo wakati wa hafla hiyo.

Rais aidha aliitaka kampuni ya KCC kupunguza gharama wanazotozwa wakulima ili kuongeza mapato yao.

Gachagua kwa upande wake alisema serikali imejitolea kuwalinda wakulima wa maziwa dhidi ya kupunjwa.

“Tutakuwa na mkutano mwezi Septemba kuangazia masuala yanayowaathiri wakulima wa maziwa,” alisema Gachagua.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *