Kenya inaunga mkono mchakato wa pamoja wa kutatua mzozo nchini Sudan.
Mapigano makali yamekuwa yakishuhudiwa Sudan yakihusisha jeshi la nchi hiyo likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kundi lenye hadhi ya kijeshi la Rapid Support Forces, RSF likiongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.
Umoja wa Mataifa, UN unasema watu zaidi ya milioni moja wamepoteza makazi nchini humo kufuatia mapigano hayo.
Wengi wamekimbilia usalama katika mataifa jirani kama vile Sudan Kusini, Misri, Chad Ethiopia.
“Kenya inaunga mkono mchakato wa pamoja wa kutatua mgogoro nchini Sudan,” alisema Rais William Ruto leo Jumatatu alipokutana na Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali, IGAD Dkt. Workneh Gebeheyu katika Ikulu ya Nairobi.
“Mtazamo ulioratibiwa unaowahusisha washikadau wote ndio fursa bora ya kurejesha amani na uthabiti, kuharakisha kurejea kwa hali ya kawaida na kuepusha janga la kibindamau nchini Sudan na eneo pana,” aliongeza Rais Ruto.
Umoja wa Afrika, AU, IGAD na Umoja wa Mataifa, UN ni mashirika ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuleta amani nchini Sudan tangu kuzuka kwa mapigano hayo mwezi Aprili mwaka huu.
Hata hivyo, jitihada zao bado hazijazaa matunda wakati uchaguzi wa kumtafuta kiongozi wa kiraia ukitarajiwa kuandaliwa nchini humo mwakani.
Hatima ya uchaguzi huo kwa kiwango kikubwa bado haijulikani.