Rais William Ruto ameilimbikizia Ujerumani sifa teletele akisema nchi hiyo imetekeleza wajibu muhimu katika kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali humu nchini.
Ametaja sekta za elimu na biashara ndogo na za kati kama ambazo Ujerumani imekuwa na mchango mkubwa.
“Kenya inakiri usaidizi ambao serikali ya Ujerumani inatoa kwa sekta ya elimu ya nchi yetu, hasa mafunzo ya kiufundi,” alisema Rais Ruto alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock katika ikulu ya Sagana.
“Natambua kwa shukrani mchango wa Ujerumani kwa biashara ndogo na za kati ambao unabadilisha kwa kiwango kikubwa maisha ya mamilioni ya Wakenya.”