Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa wakati wa utawala wake, Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA haitatawaliwa na ufisadi kama ilivyokuwa katika Bima ya Afya ya Kitaifa, NHIF.
Matamshi yake yanakuja wakati kukiwa na ripoti za mpango huo kukumbwa na ufisadi miezi michache baada kuzinduliwa kwake.
“Nataka kuihakikishia nchi kuwa changamoto za udanganyifu na ufisadi zilizokumba NHIF hazitashuhudiwa kamwe nikiwa madarakani. Hazitakuwa katika mpango wetu wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote,” amesema Rais Ruto wakati akizindua Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kilifi leo Alhamisi.
“Tumebaini gharama ya vifaa, dawa na huduma kwa kutumia wataalam. Upatikanaji wa vifaa vyovyote, vile ambavyo nasikia watu wakizingumza katika vyombo vya habari, kulikuwa na mchakato wa upatikanaji wake, ulifanywa kati ya kaunti na Wizara ya Afya, hakuna jukumu kwa kaunti yoyote kupata vifaa vyovyote kutoka kwa mtoaji huduma yoyote. Hakuna mtoaji huduma mmoja, nadhani kuna takriban watoaji huduma saba. Na hakuna jukumu lililotwikwa kaunti yoyote.”
Rais Ruto alibainisha kuwa hakuna Gavana aliyelazimishwa kutia saini mikataba ya kupata vifaa tiba katika ushirikiano huo kati ya serikali kuu na zile za kaunti.
Matamshi yake yanakuja saa chache baada ya Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa kwenye taarifa kufafanua kuhusu mpango wa kitaifa wa vifaa vya afya.
Taarifa hiyo ilifuatia makala yaliyochapishwa na gazeti moja la humu nchini kuhusu mpango huo.
Katika kusuluhisha kumalizika kwa muda wa utekelezaji wa mpango huo Disemba 2023, serikali imezindua mkakati mpya wa kuuendeleza kutokana na mafanikio ya mpango huo.
Mkakati huo uliundwa kufuatia maazimio ya kongamano la 10 lisilo la kawaida kati ya serikali za kaunti na serikali ya kitaifa Disemba 18, 2023.
Unahusisha mfumo wa kiwango kamili cha ada itakayotozwa kwa ukarabati wa vifaa unaokubalia wauzaji kuleta vifaa hivyo, kuvitunza na kuviboresha katika hospitali za kaunti bila gharama zaidi.
Mfumo huu tofauti na mfumo wa kukodisha vifaa ulioripotiwa, unahamisha jukumu la kifedha hadi kwa muuza vifaa. Unawezesha kaunti kuangazia utunzaji wa wagonjwa zikihakikisha pia uwepo wa vifaa vya kisasa zaidi.
Baraza la magavana na wizara ya afya zimesisitiza kwamba mchakato wazi wa utoaji zabuni ulitekelezwa na wakaafikia wauzaji saba Oktoba mwaka 2024.
Mapango huo mpya umeundwa kwa namna itakayouwezesha kuwa wa kufanikiwa, wazi na endelevu.
Lengo kulingana na aasasi hizo mbili za serikali ni kuimarisha utoaji huduma za afya kote nchini. Zimejitolea kuunga mkono huduma za afya kupitia mifumo shirikishi na yenye uwajibikaji.