Ruto: Uboreshaji uhusiano kati ya Kenya na India utaimarisha ajenda yetu ya maendeleo

Martin Mwanje
2 Min Read

Kenya imejitolea kuimarisha uhusiano wake wa pande mbili na India. 

Rais William Ruto amesema Kenya na India zinashirikishana uhusiano wa kihistoria ulioanza katika karne ya 18.

Ruto, ambaye anafanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini India, alisema nchi hizo mbili zinadhamiria kuboresha biashara, uwekezaji, elimu, uchumi wa dijitali, afya, utafiti na kilimo miongoni mwa nyanja zingine za ushirikiano kwa ajili ya manufaa ya watu wake.

Aidha alifanya majadiliano na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya India Exim Harsha Bangari juu ya kuanzishwa kwa makao makuu ya kikanda ya benki hiyo nchini Kenya.

Rais alisema uwekezaji kama huo ni muhimu kwa ukuaji wa kiuchumi na kijamii wa nchi hii.

“Kenya inaendelea kuvutia wawekezaji wa kigeni kutoka kila pembe ya dunia kama sehemu ya Ajenda ya Mabadiliko kuanzia Chini hadi Juu,” alisema Ruto.

Kiongozi wa nchi pia alishuhudia kusainiwa kwa mkataba wa maelewano kati ya Chuo Kikuu cha Wazi cha Kenya na Chuo Kikuu cha Wazi cha Kitaifa cha Indira Gandhi (IGNOU).

Mkataba huo unalenga kufanya kuwa anuwai programu za Kenya na kuboresha miundombinu yake ya kiteknolojia.

Kadhalika, Rais alikutana na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Procorp Enertech Private Limited, Srinivasa Raju Gannavarapu, na kuangazia fursa za uwekezaji katika Umoja wa Kiuchumi wa Kanda ya Ziwa.

Waliokuwapo ni Magavana James Orengo (Siaya), Stephen Sang (Nandi) na Hillary Barchok (Bomet) miongoni mwa wengine.

Rais Ruto pia alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India Subrahmanyam Jaishankar.

 

Share This Article