Rais wa Niger Mohamed Bazoum aliyechaguliwa kidemokrasia anapaswa kurejeshwa madarakani haraka iwezekanavyo.
Rais Bazoum aling’olewa madarakani na wanajeshi Julai, 26 mwaka huu wakitaja kuzorota kwa usalama na usimamizi mbaya wa masuala ya kijamii na kiuchumi nchini humo.
Katika kutoa wito huo, Rais Ruto amesema viongozi wa bara la Afrika wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusuluhisha masuala yanayozihusu nchi zote za bara hilo.
“Msimamo wetu ni kwamba Rais Bazoum anapaswa kurejeshwa madarakani kama Rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia na hatua yoyote ile ambayo ECOWAS itakubaliana juu yake itaungwa mkono na sisi tulio katika Umoja wa Afrika, AU ili kukomesha serikali isiyokuwa ya kidemokrasia katika bara letu,” alisema Rais Ruto.
Alikuwa akizungumza mjini Maputo nchini Msumbiji anakofanya ziara ya kitaifa ya siku mbili kuanzia jana Alhamisi.
Aliyasema hayo wakati ambapo viongozi wa Jumuiya ya Uchumi wa Afrika Magharibi, ECOWAS walikutana nchini Nigeria jana Alhamisi kuangazia hali nchini Niger.
Wakati wa mkutano huo, viongozi hao walikubaliana, miongoni mwa hatua zingine, kutuma haraka iwezekanavyo kikosi cha dharura nchini Niger kwa lengo la kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini humo na kumrejesha madarakani Rais Bazoum.
Marekani na Ufaransa ni miongoni mwa nchi ambazo zimeripotiwa kuunga mkono uamuzi wa ECOWAS.
Utawala wa kijeshi nchini Niger tayari umetangaza kuundwa kwa serikali mpya.
Mapinduzi yaliyofanyika nchini Niger mwishoni mwa mwezi Julai ni ya saba Magharibi na Katikati mwa Afrika tangu mwaka wa 2020 na wengi wanaohofia kwamba huenda yakawa na athari kubwa kwa mfumo wa demokrasia barani humo.
Mapinduzi hayo yalianzishwa na walinzi wa rais wanaotoka katika vikosi vya jeshi na kwa kawaida humlinda rais na ujumbe wake.
Viongozi wa dunia wamelaani mapinduzi hayo na kutoa wito wa kurejeshwa kwa mfumo wa kikatiba.