Waziri Mkuu wa zamani nchini Kenya Raila Odinga ana sifa zinazostahili kupigania umoja na maendeleo ya bara la Afrika.
Rais William Ruto amesema hatua ya Raila kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC inaendelea kupata uungwaji mkono mkubwa kutokana na historia yake iliyodhihirika ya kuunga mkono bara lote la Afrika.
Ameelezea imani kuwa uongozi wa Raila utasaidia kukuza amani kote barani Afrika na hivyo kudhibiti migogoro ipasavyo na kufungua uwezo wa Makubaliano ya Biashara Huru barani Africa.
“Tuna imani kuwa juhudi zilizofana za Raila za kuwania wadhifa huo zitasababisha hali ya bara letu la Afrika kubadilika na kuwa nzuri zaidi kuelekea siku za usoni,” alisema Rais.
Aliyasema hayo wakati wa toleo la nne la tamasha la kitamaduni la Piny Luo lililofanyika katika eneo la Bondo, kaunti ya Siaya leo Alhamisi.
Tamasha hilo lilihudhuriwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Museveni alisema eneo hili linaunga mkono hatua ya Raila kugombea uenyekiti wa AUC.
Raila atamenyana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf na Waziri wa zamani wa Madagascar Richard Randriamandrato kugombea wadhifa huo wakati wa uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao.