Ruto: Raila ameungwa mkono na Togo kuwania uenyekiti wa AUC

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais wa Togo Faure Essozimna Gnassingbé akiwa na Rais William Ruto

Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amepigwa jeki katika azima yake ya kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC. 

Hii ni baada ya Rais wa Togo Faure Essozimna Gnassingbé kuahidi kumuunga mkono wakati wa uchaguzi utakaoandaliwa mwezi ujao.

Rais Gnassingbé aliahidi kumuunga mkono Raila alipokutana na Rais William Ruto nchini Ghana.

Wote hao walielekea nchini Ghana kuhudhuhuria uapisho wa Rais mteule John Dramani Mahama.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Mauritius Dkt. Navinchandra Ramgoolam kuahidi kumuunga mkono Raila kugombea wadhifa huo.

Raila, aliyetimiza umri wa miaka 80 leo Jumanne, alitembelea nchi hiyo jana Jumatatu.

Uchaguzi wa uenyekiti wa AUC ambao kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki kutoka Chad umepangwa kufanywa mwezi ujao.

Raila amekuwa akitembelea nchi mbalimbali za bara la Afrika kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa bara hilo watakaopiga kura mwezi ujao kumchagua mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Raila anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf ambaye pia anapigiwa upatu kushinda wadhifa huo.

Mwingine aliye kwenye kinyang’anyiro ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *