Kuna haja ya kutafuta haraka suluhu ya kudumu kwa mgogoro unaoendelea nchini Sudan.
Mgogoro huo unaolihusisha jeshi la Sudan na kundi lenye hadhi ya kijeshi la Rapid Support Forces, RSF umesababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao.
Mgogoro huo ulikuwa kiini cha mazungumzo kati ya Rais William Ruto na Rais wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan walipokutana katika Ikulu ya Nairobi jana Jumatatu.
Rais William Ruto anasema mchakato wa Jeddah unaolenga kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro unapaswa kuharakishwa ili kusitisha uhasama nchini Sudan.
Wawili hao walikubaliana kufanya kazi kuelekea mpangokazi wa majadiliano yanayohusisha pande zote.
Wakati wa mazungumzo kati yao, viongozi hao waliangazia hali ya usalama ya hivi punde nchini Sudan na eneo hilo.
Pia walipitia upya hali ya mipango inayoendelea ya kutafuta amani, ikiwa ni pamoja na michakato ya amani ya Jeddah and IGAD.
Walisisitiza haja ya dharura ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro unaorindima nchini Sudan haraka iwezekanavyo.
Kwa mantiki hayo, Rais Ruto na Jenerali al-Burhan walikubaliana kwamba: ikizingatiwa mchakato wa Jeddah unaendeshwa kwa kasi ya kinyonga, mchakato kuelekea kusitishwa kwa uhasama na usaidizi wa kibinadamu uharakishwe na kwamba watafanya kazi kuelekea kuitishwa kwa mkutano wa viongozi wakuu wa IGAD ili kutafuta njia za kuharakisha mchakato wa Jeddah kwa lengo kusitisha uhasama nchini Sudan.
Kadhalika walikubaliana kwamba mkutano wa IGAD pia utakubali mpangokazi wa mazungumzo ya Sudan yanayozileta pamoja pande zote.
Rais Ruto aliahidi kumtaarifu mwenyekiti wa IGAD juu ya mkutano kati yake na Jenerali al-Burhan.