Rais William Ruto amesema kwamba mfumo wa elimu wa Kenya ni lazima uimarishe ujuzi, talanta na ubunifu ili kuhakikisha uwepo wa watendakazi ambao watasaidia kutekeleza maono ya kubadilisha Kenya kiuchumi.
“Ndani ya wiki chache za uongozi wangu, niliweza kubuni jopo kuhusu mabadiliko yanayohitajika katika sekta ya elimu likiongozwa na Profesa Raphael Munavu, la kuangazia mabadiliko hadi kwa mfumo wa sasa wa CBC.” alisema Rais.
Jopokazi hilo lilijukumiwa pia kutoa mapendekezo kuhusu mabadiliko yanayohitajika katika sekta ya elimu kuanzia chekechea hadi elimu ya juu.
Anasema mapendekezo kwenye ripoti ya jopo hilo tayari yanatekelezwa na swali kuu kuhusu sekondari msingi yaani Junior Secondary lilijibiwa.
Kulingana na Rais, mtihani wa kitaifa wa KPSEA sio kama mitihani ya kitaifa ya mfumo unaoondoka wa 8.4.4 bali ni wa kusaidia kujua uwezo wa mwanafunzi na maendeleo yake na wala sio wa kumwezesha kusonga hadi kiwango kingine.
Walimu 56,750 zaidi wameajiriwa huku wengine 8,200 wa shule za msingi wakipatiwa mafunzo upya ili kuweza kufundisha wanafunzi chini ya mfumo wa sasa wa elimu katika sekondari msingi.
Mabadiliko ya sekta ya elimu yamesababisha ongezeko la wanaotaka kusomea ualimu kwa kiwango cha asilimia 300 kulingana na Rais.
Pendekezo la jopokazi la sekta ya elimu katika elimu ya juu kwamba mfumo wa ufadhili ubadilishwe na kuwa wa ufadhili na wa mikopo ili kuziba mianya iliyopo tayari linatekelezwa.
Wanafunzi wa vyuo vikuu na wa taasisi za mafunzo ya kiufundi wanapata ufadhili na mikopo ya elimu kulingana na mahitaji.
Alifafanua kwamba elimu ya juu sasa inapatikana kwa wote hasa kupitia kubuniwa kwa chuo kikuu cha wazi yaani Open University of Kenya baada ya kuidhinishwa na bunge na baraza la mawaziri.