Ruto: Mapendekezo ya mabadiliko katika sekta ya usalama kuanza kutekelezwa mara moja

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba mabadiliko yaliyopendekezwa na jopokazi kuhusu mabadiliko katika maslahi ya maafisa wa usalama yanafaa kuanza kutekelezwa mara moja.

Akizungumza katika ikulu ya Nairobi alipopokea rasmi ripoti ya jopokazi hilo, kiongozi wa nchi alisema mapendekezo yaliyomo ni bora na hayafai kucheleweshwa hata kidogo.

Rais Ruto alisifia ripoti ya jopo hilo akisema imeafikia malengo yake kwa sababu wanachama walikuwa wamejitolea kikamilifu na walikuwa wakimjuza kila mara kuhusu hatua walizopiga.

Kiongozi wa nchi alisema kulingana na ripoti hiyo matatizo makubwa katika sekta ya ulinzi ni ufadhili, uongozi mbaya, mifumo hafifu ya usimamizi na ufisadi.

Matatizo hayo kulingana naye, yamesababisha maafisa wa usalama kukosa motisha wa kazi na anaamini yakisuluhishwa, watajitolea kikamilifu kulinda maisha na mali ya wakenya.

Alisema serikali itaangazia kwa makini mapendekezo ya jopo hilo ambapo mengine yatatekelezwa mara moja huku yanayohitaji kuidhinishwa na bunge yakisubiri kwa muda.

Kwa sababu hiyo masharti ya kikazi ya maafisa wote wa usalama yataboreshwa ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara yao, kuwapa bima faafu ya afya, kuhakikisha wana makazi bora kati na maslahi mengine.

Rais William Ruto aliunda jopokazi hilo kuhusu mabadiliko katika maslahi ya maafisa wa usalama Disemba mwaka 2022 kwa lengo la kuimarisha utendakazi wao.

Jopo hilo la wanachama 20 liliidhinishwa kupitia kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali Alhamisi Disemba 22, 2022.

Jaji mkuu mstaafu David Maraga amekuwa akiongoza jopo hilo kama mwenyekiti huku Carole Kariuki akiteuliwa kuwa naibu mwenyekiti.

Share This Article