Nambari zote za paybill zinazotumiwa kwa sasa kulipia huduma za serikali zitafutiliwa mbali katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Rais William Ruto amesema baada ya kufungwa kwa nambari hizo, malipo yote kwa huduma za serikali yatatolewa kupitia nambari moja tu ya paybill: nayo ni 222 222.
Malipo yote yatakayofanywa kupitia nambari hiyo yataelekea kwa Wizara ya Fedha ambayo ndio mmiliki.
“Tuna tatizo la baadhi ya nambari za paybill ambazo hatuwezi tukawajibikia, tuna zaidi ya nambari 1,000 za paybill kila mahali zinazoendeshwa na watu ambao hata hatuwafahamu,” alisema Rais Ruto katika jumba la KICC wakati wa uzinduzi wa programu ya Gava Mkononi itakayohakikisha Wakenya wananufaika na huduma za serikali kupitia mfumo wa kidijitali wa e-Citizen katika jumba la KICC, Nairobi.
“Hatua hii itahakikisha Wizara ya Fedha inafuatilia na kubaini huduma mbalimbali zinazolipiwa na watumiaji.”
Hii ni njia moja ambayo serikali inakusudia kuboresha ukusanyaji ushuru kwa lengo la kufadhili bajeti na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya serikali kote nchini.
Rais Ruto, , alisema kufikia mwishoni mwa mwaka huu, huduma zote karibu 10,000 za serikali zinapaswa kupatikana kwa njia ya dijitali kupitia mfumo wa e-Citizen.
Aliongeza kuwa serikali inaweka vituo 25,000 vya hotspots kote nchini kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa huduma hizo.