Wakenya watakiwa kujitokeza kwa wingi kupanda miti

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto Jumatatu ijayo atazindua zoezi la upanzi wa miti kote nchini katika eneo la Makindu, kaunti ya Makueni. 

Serikali imetangaza Novemba 13 kuwa sikukuu ya upanzi wa miti.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo anatoa wito kwa Wakenya kote nchini kujitokeza kwa wingi na kuwa katika mstari wa mbele kwa upanzi wa miti siku hiyo.

“Wakenya wanaombwa kufika ofisi ya Chifu iliyo karibu nao kuchukua miche na kushirikiana na Naibu Kamishna wa Kaunti katika kaunti zao husika,” anasema Dkt. Omollo katika taarifa.

Katika ngazi ya kaunti, shughuli za upanzi wa miti zitaongozwa na mawaziri katika angalau kaunti mbili, wakishirikiana na Magavana husika na kuungwa mkono na Makatibu, Makamishna wa Kaunti na maafisa wengine waandamizi serikalini.

Maafisa wa utawala wa serikali kuu wataisaidia Wizara ya Mazingira katika kufanikisha zoezi hilo kuelekea utimizaji wa lengo la serikali la upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

“Makamishna wa kaunti tayari wameunda timu za mipango za kiufundi katika kaunti zao husika zikiwajumuisha wawakilishi kutoka Huduma ya Misitu ya Kenya, KFS na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, NEMA miongoni mwa washikadau wengine wa serikali na wasiokuwa wa serikali,” anasema Dkt. Omollo.

 

 

Share This Article