Serikali ya Kenya Kwanza imeweka mikakati kabambe inayodhamiria kuhakikisha nchi hii haiagizi kabisa chakula katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Rais William Ruto amesema serikali inakusudia kupunguza uagizaji chakula kwa asilimia 59.
“Shilingi bilioni 500 ambazo tunatumia kila mwaka kuagiza chakula zinaweza tu kupunguzwa siku ambayo tutazalisha chakula nchini Kenya,” alisema Rais Ruto wakati akiwahutubia wanahabari mjini Naivasha leo Jumatano.
“Hio ndio hatua tunayoichukua, na tumetoa ahadi kama serikali kwamba tunataka kupunguza uagizaji chakula kwa asilimia 50 katika kipindi cha miaka mitano ijayo na kwa asilimia 100 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.”
Mathalan, Rais Ruto anasema katika kipindi hicho cha miaka 10, Kenya haitaagiza mafuta ya kupikia, sukari na mahindi.
https://twitter.com/i/status/1760248335930159452
Tangu ilipoingia madarakani, serikali ya Kenya Kwanza imeelekeza jitihada zake katika kupiga jeki uzalishaji wa chakula nchini kupitia mpango wa utoaji wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima.
Kupitia mpango huo, serikali inakusudia kuhakikisha wakulima wanazalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya nchi na hivyo kuiepushia nchi shari ya kuagiza bidhaa kama vile mahindi na sukari kama ambavyo imeshuhudiwa miaka iliyopita.