Rais William Ruto ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuifanyia mabadiliko mifumo iliyopitwa na wakati iliyo na mamlaka na ushawishi duniani.
Badala yake ameitaka jumuiya hiyo kubuni mfumo wa ushirikiano wa kimataifa unaoakisi matamanio na uadilifu wa kila binadamu.
“Ni lazima tuwe na maono mapya ya umoja wa dunia, ule unaodumisha kanuni za usawa na jumuishi,” alisema Rais Ruto wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Alhamisi mjini New York nchini Marekani.
“Ili kufikia hili, Kenya inatoa wito wa mifumo ya fedha duniani kufanyiwa mabadiliko, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, upanuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuijumuisha Afrika na uharakishaji wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.”