Ruto awataka wabunge kuunga mkono mswada wa nyumba za bei nafuu

Martin Mwanje & PCS
2 Min Read
Rais William Ruto ametoa wito kwa wabunge kuunga mkono mswada wa nyumba za bei nafuu na kusaidia kuwatafutia vijana ajira.
Ruto amewataka wabunge kuchukua mtazamo wa pande mbili wakati wa mjadala na uidhinishaji wa mswada huo katika bunge la taifa siku ya Jumatano.
Amesema mpango wa nyumba za bei nafuu utatoa fursa za ajira kwa vijana zaidi ya 300,000 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Kulingana naye, tayari vijana 130,000 wanafanya kazi katika maeneo mbalimbali ya ujenzi kote nchini.
“Hii haihusiani na vyama vya kisiasa; siyo kati ya walio navyo na walala hoi. Hii inahusu fursa za ajira kwa ajili ya mamilioni ya Wakenya wanaofanya kazi katika sekta ya ujenzi na sekta husika za uongezaji thamani,” aliongeza Rais Ruto.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu 220 za mradi wa Makenji katika eneo la Kandara, kaunti ya Murang’a. Mradi huo utabuni nafasi za ajira zaidi ya 1,600 na kupanua nafasi kwa ajili ya wakazi.
Rais Ruto alitumia fursa hiyo kusisitiza dhamira ya serikali kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini.
Alitaja kuanzishwa kwa vituo vya teknolojia ya habari na mawasiliano, ICT katika kila wadi 1,450 nchini akisema vitasaidia kubuni maelfu ya ajira za kidijitali na kupeleka wafanyakazi Wakenya nje ya nchi.
Kwa upande wake, Naibu Rais Rigathi Gachagua alielezea imani kuwa uchumi wa nchi unaimarika, akitoa mfano wa kuimarika kwa shilingi ya Kenya dhidi ya dola.
Alisema Rais Ruto anatimiza ahadi zake kwa Wakenya licha ya nyakati ngumu za kiuchumi.
Martin Mwanje & PCS
+ posts
Share This Article