Rais William Ruto ametoa onyo kali kwa wakandarasi wanaochelewesha utekelezaji wa miradi muhimu ya serikali.
Ruto amesema serikali imekusudia kutimiza ahadi zake kwa raia, akiongeza kuwa kuhujumu juhudi zao hakutavumiliwa.
“Kuna wakandarasi wengi wanaotuangusha, na hatutawakubalia. Huu ni mwaka wa kutimiza ajenda yetu kama ilivyopangwa ,” alisema Rais.
Ruto aliyasema hayo leo Jumatano mjini Kisii ambako alikagua ujenzi wa Kituo cha Saratani cha Kisii.
Alielezea kutoridhishwa na hatua iliyopigwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Rais Ruto alimwagiza mkandarasi huyo kutekeleza mradi huo kulingana na inavyotaka serikali la sivyo kandarasi hiyo ifutwe.
“Umelipwa fedha zote zilizohitajika. Hakuna sababu ya mradi huu kutosonga mbele.”