Rais William Ruto ametoa hakikisho kuwa uwanja mpya unaojengwa wa Talanata City Sports Complex utakamilika kwa wakati ufaao ili kuanda fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Ruto amesema haya Jumapili jioni katika uwanja wa taifa wa Nyayo alipokuwa mgeni wa heshima katika sherehe za klabu ya AFC Leopards iliyoadhimisha miaka 60 tangu ibuniwe.
Alipongeza mchango wa vilabu vya kijamii katika ukuzaji wa soka humu nchini akitaja timu kama vile Leopards, Gor Mahia na Shabana FC katika kujenga historia.
Rais alitoa mchango wa shilingi milini 10 kwa Ingwe huku Waziri wa Michezo Ababu Namwamba na Gavana wa Nairobi Jonshon Sakaja wakitoa shilingi milioni 2 kila mmoja.
Magavana Simba Arati wa Kisii na mwenzake wa Bungoma Ken Lusaka na Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, walitoa mchango wa shilingi milioni moja kila mmoja naye mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi akaongezea shilingi nusu milioni.
Rais pia alihudhuria mechi mbili za kirafiki kati ya AFC Leopards na klabu ya AE Ramassa ya daraja la nne kutoka Uhispania ambazo Ingwe walisajili ushindi wa mabao 2-1 na 4-3.
Lengo kuu la klabu hiyo ni kubadilishwa kutoka klabu ya kijamii hadi kuwa kampuni ili kujitosheleza kifedha.
Leopards iliyozinduliwa Machi 12 mwaka 1964, wametwaa ubingwa wa ligi kuu ya Kenya mara 12.