Rais William Ruto amezitaka idara za upelelezi kuchukua hatua za haraka na kukomesha mauaji ya wanawake yanayoongezeka nchini.
Ripoti zinaonyesha kuwa wanawake zaidi ya 90 wameuawa katika kipindi cha miezi mitatu tu iliyopita.
Ruto anasema kuna haja kwa Idara ya Upelelezi, DCI kwa kushirikiana na idara zote za uchunguzi kuhakikisha wahalifu wanaotekeleza mauaji hayo wanakabiliwa na mkono mrefu wa sheria.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kwa Naibu Rais Prof. Kindiki katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC leo Ijumaa, Rais Ruto pia amewataka Wakenya kujiepusha na watu wasowafahamu ambao yamkini wanakusudi la kutekeleza maovu kama hayo katika jamii.
“Najua katika siku za hivi karibuni, tumeona visa vya wasichana wetu, kina mama wetu, wanawake wetu ambao wameuawa kikatili. Na hebu niseme hivi, kwamba DCI na mamlaka zote za uchunguzi katika Jamhuri ya Kenya lazima zikabiliane na wahalifu hawa,” aliagiza Rais Ruto.
Jaji Mkuu Martha Koome ni miongoni mwa wale ambao wamelaani mauaji hayo wakitaka hatua za haraka zichukuliwe.
Koome amesema mauaji hayo sio tu jinai bali pia ni vitendo vya kinyama na familia za waathiriwa zinapaswa kupata usaidizi kwani zinapitia wakati mgumu.
Maoni kama hayo yametolewa na Chama cha Wanawake Mawakili nchini, FIDA.