Ruto asaini Mswada wa Matumizi ya Fedha 2024

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto leo Ijumaa ametia saini Mswada wa Matumizi ya Fedha 2024 ili kuhakikisha shughuli za serikali zinaendelea kama kawaida. 

Kwa mujibu wa katiba, mswada huo unapaswa kutiwa saini kufikia Juni 30 kila mwaka.

Hata hivyo, Rais Ruto ameiagiza Wizara ya Fedha kuandaa makadiro ya ziada mara moja ili kupunguza matumizi ya fedha za serikali kwa kiasi cha mapato ambacho kingetokana na Mswada wa Fedha 2024 uliokataliwa.

Jumla ya shilingi bilioni 346 zilitarajiwa kukusanywa kupitia kwa mswada huo kwa njia ya kodi.

Serikali za kuu na serikali za kaunti sasa zitalazimika kwa usawa kutafuta njia ya kuziba nakisi hiyo iliyotokana na kukataliwa kwa mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Katika taarifa, Rais Ruto aliyetia saini Mswada wa Matumizi ya Fedha 2024 leo Ijumaa amesema serikali kuu itaziba nakisi hiyo kwa kupunguza matumizi ya fedha za serikali kuu, bunge, idara ya mahakama na tume zingine za kikatiba.

Kwa misingi hiyo, Rais amerejesha bungeni Mswada wa Ugavi na Mapato ya Kaunti uliojikita kwenye mapato yaliyotarajiwa kukusanywa kupitia kwa Mswada wa Fedha 2024 uliokataliwa. Matumizi ya fedha katika mswada huo sasa yanatarajiwa kupunguzwa ili kuakisi ukweli wa mambo yalivyo sasa.

Kadhalika, Rais ameiagiza Wizara ya Fedha kuwasilisha bungeni mara moja marekebisho kwa Sheria ya Ugavi wa Mapato 2024 ili kuakisi mapato yaliyopunguzwa kutokana na kukataliwa kwa mswada wa fedha.

Hadi bajeti ya ziada itakapoidhinishwa, Wizara ya Fedha pia imetakiwa kuwaagiza mahasibu kuhakikisha kuwa hi huduma muhimu pekee zinazofadhiliwa kwa kutumia fedha zisizozidi asilimia 15 ya bajeti.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *