Rais William Ruto amesaini kuwa sheria miswada minne ya upatikanaji wa afya kwa wote.
Miswada iliyotiwa saini na Rais ni pamoja na Mswada wa Bima ya Afya kwa Jamii 2023, Mswada wa Utoaji Huduma za Msingi za Afya 2023, Mswada wa Afya ya Dijitali 2023 na Mswada wa Ufadhili wa Uboreshaji wa Vituo vya Afya 2023.
Hafla ya utiaji saini miswada hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Alhamisi na kuhudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Maspika Moses Wetang’ula wa bunge la Taifa na Amason Kingi wa bunge la Seneti na magavana miongoni mwa viongozi wengine.
“Leo, miswada minne muhimu ya utekelezaji wa afya kwa wote imekuwa sheria. Sheria hizi, pamoja na sera na mikakati mingine mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sera ya afya kwa jamii, afya ya msingi na mikakati ya ufadhili wa afya itaweka msingi kwa mabadiliko makubwa katika mfumo wetu wa afya tangu uhuru,” alisema Rais Ruto.
Serikali imeelezea matumaini kuwa miswada hiyo itasaidia katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kote nchini huku wahamasishaji wa afya katika jamii wakitarajiwa kutekeleza wajibu muhimu.
Miswada hiyo imesainiw akuwa sheria siku moja kabla ya kuandaliwa kwa Siku ya Mashujaa ambayo kaulimbiu yake ni upatikanaji wa afya kwa wote.
Sherehe za siku hiyo zitafanyika katika uwanja wa michezo wa Kericho Green katika kaunti ya Kericho kesho Ijumaa.