Ruto amtembelea Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta Gatundu

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumatatu amemtembelea mtangulizi wake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta nyumbani kwake huko Gatundu. 

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed, wakati wa ziara hiyo, wawili hao walizungumzia masuala mbalimbali muhimu ya kitaifa na kikanda.

Ruto kadhalika alimshukuru Uhuru kutokana na alivyoongoza vizuri mchakato wa ubadilishanaji wa madaraka na kwa jinsi anavyoendelea kuunga mkono utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo humu nchini.

“Viongozi wote wawili walitambua kuwepo kwa mazingira yenye changamoto duniani yanayoathiri nchi nyingi, ikiwemo Kenya, yaliyosababishwa na vigezo malimbali: athari za COVID-19, vita nchini Ukraine – vilivyoathiri mitungo ya usambazaji na kusababisha kupanda kwa bei za bidhaa, hasa mbolea na mtama – soko linaloyumba la fedha na hali mbaya ya kiuchumi,” ilisema taarifa ya Msemaji wa Ikulu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ruto pia alimshukuru Uhuru kwa kuweka msingi thabiti wa nchi ambao umeiwezesha serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza Ajenda yake ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu (BETA).

Na huku serikali ya Kenya Kwanza ikilaumiwa kwa kuchelewesha uundaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), viongozi hao wawili pia walizungumzia suala hilo. Wawili hao wakitoa wito wa kesi zilizopo mahakamani kusuluhishwa haraka ili kupisha kuteuliwa kwa makamishna wa tume hiyo.

Mjadala juu ya kukawia kuwateua makamishna wa IEBC ulitifuliwa na Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola aliyewanyeshea wabunge kidole cha lawama kwa kuipa IEBC kisogo katika upitishaji wa sheria bungeni.

Tangu wakati huo, Wakenya wamekuwa wakishinikiza kuteuliwa kwa makamishna wa IEBC ili kuiepushia nchi janga la kikatiba siku zijazo.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *