Rais William Ruto amefanya kikao cha faragha na Seneta Chris Coons wa Marekani katika ziara yake mjini New York.
Seneta Coons anayewakilisha jimbo la Delaware amezuru Kenya mara kadhaa na wakati wa ziara yake nchini, alikutana na Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Coons amekuwa mstari wa mbele kutoa wito kwa viongozi hao wawili kukumbatia moyo wa majadiliano katika kutatua masuala yanayolikumba taifa.
Wakati wa mkutano baina yao, Rais Ruto alikariri kujitolea kwa serikali yake kuimarisha ushirikiano thabiti, utakaowezesha ukuaji wa biashara na fursa za uwekezaji.
Rais Ruto yupo nchini Marekani kuhudhuria kongamano la kimataifa.
Akiwa nchini, Marekani Ruto amekutana pia na washirika mbalimbali wa kampuni kubwa za kiteknolojia kama vile Google katika jitihada za kuwashawishi kuwekeza nchini Kenya au kuongeza kiwango cha uwekezaji.