Ruto akutana na Naibu Katibu Mkuu wa UN, wazungumzia amani na usalama duniani

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto wakati wa mkutano na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Amina J. Mohammed

Rais William Ruto leo Jumatano asubuhi amekutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Amina J. Mohammed katika Ikulu ya Mombasa. 

Wakati wa mkutano kati yao, wawili hao walizugumzia masuala ya usalama na uthabiti duniani, huku hali katika nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Sudan zikijadiliwa.

“Tulizungumzia hali mashariki mwa DRC na hatua kubwa iliyopigwa na michakato ya pamoja ya amani ya EAC-SADC, ikiwa ni pamoja na kuteuliwa kwa wapatanishi wa kuongoza juhudi za amani na hatua za kurejesha uthabiti,” alisema Rais Ruto baada ya mkutano kati yao.

“Pia tuliangazia mgogoro unaosababisha maafa nchini Sudan na umuhimu wa kuchukua hatua za dharura za kutumia fursa zote zilizopo kufanya mazungumzo na utatuzi wa amani wa mzozo huo.”

Aidha, Rais Ruto na mgeni wake walizungumzia changamoto za kiusalama zinazoshuhudiwa nchini Haiti na msaada unaotolewa na UN katika kusaidia kuzisuluhisha.

Kiongozi wa nchi akitumia fura hiyo kuipongeza dhamira ya UN ya kuisaidia Kenya katika kuongoza Kikosi cha Kimataifa cha Kudumisha Usalama nchini Haiti (MSS).

Kenya imetuma zaidi ya maafisa 900 wa polisi ambao ni sehemu ya kikosi hicho kinachokabiliana na magenge ya wahalifu yanayolihangaisha taifa hilo la Caribbean.

Afisa mmoa wa polisi wa Kenya ameripotiwa kufariki katika operesheni ya usalama nchini humo.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *