Ruto akagua na kuahidi miradi ya maendeleo Migori

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, Ruto amekita kambi katika eneo pana la Magharibi mwa nchi ambako anakagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto aliendelea na ukaguzi wake wa miradi ya maendeleo katika eneo la Nyanza, wakati huu akielekea katika kaunti ya Migori. 

Akiwa ameandamana na Gavana wa kaunti hiyo Ochillo Ayacko, Ruto alikagua kazi za ujenzi zinazofanywa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kegonga katika eneo bunge la Kuria Mashariki.

Mradi huo unaokusudiwa kuhakikisha upatikanaji wa afya bora kwa wakazi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 345.

“Tutawekeza shilingi milioni 150 kwa ujenzi wa nyumba za wanafunzi kuishi katika Chuo cha Mafunzo ya Utabibu cha Kegonga KMTC ili kuunga mkono utoaji mafunzo na ujenzi wa makazi ya wanafunzi wa utoaji huduma za matibabu,” aliahidi Ruto.

“Pia tutajenga soko la kisasa litakalogharimu shilingi milioni 200 ili kuimarisha biashara na ukuaji uchumi wa mji wa Kegonga.”

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kiongozi wa nchi amekuwa na pirikapirika nyingi katika eneo pana la Magharibi mwa nchi, ambako amezindua miradi ya maendeleo katika kaunti za eneo hilo ikiwa ni pamoja na Kakamega, Busia, Bungoma na Vihiga.

Kisha baada ya hapo, alizindua ujenzi wa reli ya kisasa SGR katika kaunti ya Narok na Kisumu kabla ya kukita kambi katika kaunti za eneo la Nyanza anakoendelea kuzindua miradi ya maendeleo.

Wachambuzi wanasema mbali na kuzindua miradi hiyo, Ruto analenga kuitumia kama chambo cha kupata uungwaji mkono wa wakazi wa eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article