Ruto aapa kuangamiza matapeli katika sekta ya mafuta

Ameahidi hilo siku moja baada ya kujiuzulu kwa Katibu wa Idara ya Petroli Mohamed Liban na Wakurugenzi Wakuu Joe Sang wa Kenya Pipeline na Daniel Kiptoo wa EPRA.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ametoa onyo kali huku akiapa kutokomeza matapeli katika sekta ya mafuta nchini. 

Ruto ameapa kufanya hivyo siku moja baada ya maafisa watatu wakuu katika sekta hiyo kujiuzulu kwa tuhuma za kuagiza mafuta ya kiwango cha chini.

“Hawa cartels wa mambo ya mafuta, watakipata. Hawawezi kuhepa kwa sababu haiwezekani katika taifa letu la Kenya watu waone tuko na shida ya Middle East, wanajaribu kukoroga shida nyingine hapa Kenya,” alionya kiongozi wa nchi.

“Hivyo nataka niseme waziwazi, huu ndio utawala ambao utakabiliana vikali na vilivyo na matapeli wote. Hii Kenya, nilisema pale mwanzo ya kwamba hatutaongeza juu ya mambo ya ufisadi. Tutafanya yale ambayo inatakikana ifanywe ndio ufisadi ikomwe katika taifa letu la Kenya. Watu walifikiri ni mchezo, wengine wakifikiria ni mzaha,” aliongeza kiongozi wa nchi.

Ruto alitoa mfano wa matapeli waliotawala awali katika sekta ya kilimo wakiwauzia Wakenya mawe kwa kusingizia kuwa ni mbolea huku wengine wakitamalaki  sekta za sukari na kahawa kabla ya kukabiliwa vikali na mkono mrefu wa sheria wa serikali.

Jana Jumamosi, Katibu wa Idara ya Petroli Mohamed Liban, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kenya Pipeline Joe Sang na Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) Daniel Kiptoo Bargoria walitangaza kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya uagizaji mafuta ya ubora wa kiwango cha chini hapa nchini.

Kwenye taarifa, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei alisema wa awali unaashiria kuwa maafisa waliojukumiwa na usimamizi wa usambazaji bidhaa za petroli, wamevuruga data ya hifadhi ya mafuta kuashiria kuwa kuna upungufu wa mafuta hapa nchini.

“Rais amesikitika kuwa wale waliojukumiwa kusimamia mfumo wa usambazaji mafuta, wamevuruga data kuhusu kiwango cha mafuta kinachohifadhiwa. Hatua hii huenda ilitekelezwa kutokana na ongezeko la mafuta duniani, na hivyo kubuni dhana potovu kuna upungufu wa mafuta,” alisema Koskei kwenye taarifa hiyo.

 

 

 

 

 

Share This Article