Ruth Kadiri ambaye ni mwigizaji wa filamu za Nollywood nchini Nigeria, amewafokea waandaaji filamu ambao hushinikiza waigizaji wao kuhakikisha filamu zao zinatazamwa kwa wingi mitandaoni katika muda mfupi.
Kadiri kupitia akaunti yake ya Instagram, Kadiri alisema kwamba mahitaji kama hayo hayana msingi kama vile kuwataka filamu zao zitazamwe zaidi ya mara milioni moja kwa siku kwenye majukwaa kama vile You Tube.
Kulingana na mwigizaji huyo ambaye pia hujihusisha na uandaaji filamu, waandaaji wengine wameshindwa na kazi zao na sasa wanawatwika mzigo waigizaji.
Aliwataka waigizaji wajiondolewe madhila kwani filamu nzuri inahitaji zaidi ya sura ya mwigizaji ili kuafikia mauzo.
Kadiri alisema pia kwamba kutazamwa mara milioni moja kwenye You Tube sio ishara au kiwango cha mafanikio au kushindwa na kwamba kuna mengi ambayo watu hawafahamu kuhusu YouTube.
Aliwatia moyo waigizaji akiwashauri wasikubali kushinikizwa na waandaaji filamu wanaolenga kuwapokonya furaha maishani.