Aliyekuwa waziri wa fedha Henry Rotich na wenzake wanane wameondolewa makosa kwenye kesi ya ufisadi ya shilingi Bilioni 63 ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.
Hakimu Eunice Nyutu akitangaza kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo leo alisema kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuongoza kesi hiyo.
Alisema pia kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kuonyesha kwamba waziri huyo wa zamani na wenzake wanane walikosa kufuata taratibu za manunuzi kwenye kesi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.
Mwezi jana, Rotich aliomba mahakama imwondolee lawama kwenye kesi hiyo akisema kwamba dhana ya pesa za mabwawa hayo mawili kupotea au kuibwa sio ya ukweli.
Aliendelea kujitetea mbele ya mahakama kudhihirisha haja ya kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo akisema kwamba upande wa mashtaka ulikosa kuwasilisha mashahidi kimakusudi.
Kupitia kwa wakili wake Kioko Kilukumi, Rotich alisema amekuwa mtendakazi wa umma kwa zaidi ya miaka 25 na kuwa waziri wa kwanza wa fedha chini ya katiba mpya na alifanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea.
Mwezi Septemba mwaka huu hakimu mkuu wa kukabiliana na ufisadi Eunice Nyutu alilalamikia jinsi afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ilikuwa ikiendesha kesi hiyo ambapo alidai kwamba maafisa wasiojulikana walikuwa wameacha kesi hiyo katika hali ya kutatanisha.
Wakati huo alikosa kuhitimisha kesi hiyo huku akiinyoshea kidole cha lawama afisi hiyo ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma akielezea kwamba maafisa fulani wa afisi hiyo walikuwa wanashinikiza viongozi wa mashtaka kutupilia mbali kesi hiyo.
Alisema kutojitolea kwa afisi hiyo kuendelea kesi hiyo kulimsababishia matatizo huku akielekeza viongozi wa mashtaka kufikisha mashahidi mahakamani.