Mwigizaji wa muda mrefu wa filamu za Nigeria Richard Mofe-Damijo almaarufu RMD ametaja uteuzi wake kujiunga na bodi ya akademia inayofahamika kwa tuzo za Oscar kuwa zawadi nzuri ya siku yake ya kuzaliwa. Nguli huyo alizaliwa tarehe 6 Julai na anatimiza umri wa miaka 62.
Damijo ni mmoja wa wahusika wa sekta ya filamu nchini Nigeria inayofahamika sana kama Nollywood ambao wameteuliwa kujiunga na bodi ya Oscar. Wengine ni mwelekezi wa filamu CJ Obasi, mtayarishaji filamu Jade Osiberu na waandishi wa miswada ya filamu Kunle Afolayan na Shola Dada.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Damijo alisema kwamba alikuwa amepokea jumbe za kumpongeza hata kabla ya kuthibitisha uteuzi wake. Anasema wanaomsimamia kama mwigizaji hatimaye walithibitisha na sasa anashukuru kwa jumbe hizo. “Sifahamu waliochangia uteuzi huo lakini ninashukuru sana kwa kunitambua.” aliandika Mofe.
Uteuzi wa watano hao unamaanisha kwamba sasa watapatiwa haki za kupiga kura katika uteuzi wa wawaniaji wa tuzo za Oscar na washindi.
Kupitia ujumbe kwenye tovuti ya akademia hiyo, mkurugenzi mkuu Bill Kramer na rais Janet Yang walikaribisha watano hao kutoka Nollywood wakisema kwamba wanawakilisha talanta za ubora wa hali ya juu ulimwenguni katika sekta ya filamu na kuchangia katika sanaa na sayansi ya filamu.
Awali akademia hiyo ilijipata pabaya pale iliponyoshewa kidole cha lawama kwa kukosa uwakili unaohitajika. Mwaka 2012 utafiti wa gazeti la Los Angeles Times ulibainisha kwamba asilimia 94 ya wapiga kura katika tuzo za Oscar ni wazungu.
Tuzo za Oscar huchukuliwa kuwa tuzo kubwa zaidi ulimwenguni ambazo hutambua na kutuza talanta katika sekta nzima ya filamu.