Mwigizaji wa muda mrefu wa filamu za Nigeria Rita Edochie ambaye ni shangazi ya mwigizaji Yul Edochie amemkosoa Nabii Odumeje kwa kuruhusu Yul na mkewe wa pili Judy Austin kusimama kwenye madhabahu ya kanisa lake.
Haya yanajiri baada ya video kusambazwa mitandaoni ikimwonyesha Yul na Judy wakiwa wamesimama kwenye madhabahu kuhutubia waumini.
Yul anasikika akijimiminia sifa pamoja na mkewe Judy, jambo ambalo lilimghadhabisha Rita ambaye anampendelea mke wa kwanza wa Yul aitwaye May.
Rita ambaye awali alimuunga mkono Odumeje kwa dhati sasa anaelezea masikitiko yake kuhusu hatua ya Nabii huyo ya kuruhusu wawili hao kusimama kwenye madhabahu.
Kulingana naye, wanandoa hao wawili sio wasafi kiroho na madhabahu ni eneo takatifu. Huwa anamtupia Judy maneno mara kwa mara mitandaoni kwa kile anachokitaja kuwa kuharibu ndoa ya May na Yul.
“Ninamlaumu nabii wangu na babangu wa kiroho kwa kukubalia sarakasi hii iendelee. Sitaki kusema nimesikitishwa na kilichotokea. Kwenye madhabahu ambayo wakati mmoja niliyaheshimu sana.” aliandika mama huyo.