Mwanahabari wa Shirika la Utangazaji hapa nchini (KBC) Fredrick Parsayo, ameaga dunia.
Habari za kifo chake, zilitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Agnes Kalekye leo Ijumaa.
Mwanahabari huyo alifariki katika njia tatanishi nyumbani kwake mtaani Kinoo, eneo bunge la Kikuyu kaunti ya Kiambu. Maafisa wa polisi wanachunguza kifo hicho.
“Tunasikitika kuwafahamisha kuhusu kifo cha Fredrick Parsayo, ambaye ni ripota katika chumba chetu cha habari, kilichotokea Ijumaa Machi 21, 2025 katika hali tatanishi. Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Kikuyu,” ilisema taarifa ya Mkurugenzi huyo Mkuu.
Kalekye alituma risala za rambirambi kwa jamaa ndugu na marafiki wa Parsayo, wakati huu mgumu wa majonzi.
“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, wasimamizi na wafanyakazi wote, tunatuma risala za rambirambi kwa marafiki na familia ya Parsayo na wale wote walioathiriwa na kifo chake. Mawazo yetu yako nanyi wakati huu mgumu,” alisema Kalakye.
Mwili wake unahifadhiwa katika makafani ya St. Teresa.