Declan Rice, alipachika mabao mawili naye Mikel Merino, akaongeza moja na kuwasaidia wenyeji Arsenal, kuwacharaza mabingwa watetezi Real Madrid mabao 3-0, katika duru ya kwanza ya kwota fainali Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku ugani Emirates.
Mechi hiyo iliishia sare tasa kunako kipindi cha kwanza, kabla ya Rice, kufungua ukurasa wa karamu ya magoli kunako dakika ya 58 na kuongeza la pili dakika ya 70 kupitia mikwaju ya ikabu.
Merino alihitimisha kazi kwa washika bunduki kwa bao la tatu dakika ya 75, huku wakisubiri mkondo wa pili Jumatano ijayo katika uchanjaa wa Santiago Bernabeu.
Bayern wakicheza nyumbani Alianz, waliambulia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa miamba wa Italia, Intermilan.
Lautaro Martinez na Davide Frattesi, walipachika magoli ya wageni Inter, huku mzee wa kazi Thomas Muller, akifunga la kufutia machozi kwa wenyeji.
Mechi mbili za mwisho kupigwa leo usiku, Barcelona ikiwaalika Borussia Dortmund ya Ujerumani, nayo Aston Villa izuru Parc De Princes dhidi ya Paris St Germain ya Ufaransa.