Reno Omokri azungumzia hatua ya Rais wa Burkina Faso ya kujihami nchini Ghana

Rais Ibrahim Traoré alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais Mahama wa Ghana akiwa amebeba bunduki yake, tofauti na alivyofanya alipokutana na Rais Vladmir Putin wa Russia

Marion Bosire
2 Min Read

Reno Omokri ambaye ni mwandishi wa vitabu na mchambuzi wa masuala ya utawala ametoa maoni yake kuhusu hatua ya Rais wa Burkina Faso Ibrahim Traoré, ya kubeba bunduki yake hadi alipokutana na Rais wa Ghana John Dramani Mahama.

Traoré alikuwa mmoja wa viongozi wa mataifa ya Afrika waliohudhuria hafla ya uapisho ya Rais Mahama jijini Accra nchini Ghana na kama kawaida alifika huko akiwa na mavavi rasmi kama mwanajeshi na bunduki yake.

Omokri alichapisha picha ya wakati Traore alikutana na Rais wa Urussi Vladimir Putin bila silaha na nyingine alipokutana na Rais Mahama jana akiwa na bunduki yake kiunoni.

Anasema wa kulaumiwa sio Traore bali ni maafisa wa itifaki wa taifa la Ghana, akisema wangemshurutisha aache silaha hiyo au wamzuie asihudhurie hafla hiyo.

“Rais Obasanjo aliwahi kufanya hivyo na Kanali Muammar Gaddafi jijini Abuja. Gaddafi alipokataa kuacha silaha yake katika uwanja wa ndege wa Abuja Jumanne Novemba 28,2006, Obasanjo aliingilia kati na Gaddafi alipoona amezidiwa alikubali kuachia silaha yake.” ameandika Omokri.

Kulingana naye, wasimamizi wa itifaki wa Rais Mahama walistahili kuchukua hatua sawia na iwapo wangeshindwa, Mahama mwenyewe angeingilia kati.

Omokri raia wa Nigeria wa umri wa miaka 50 sasa aliendelea kuelezea jinsi taifa la Russia liko makini sana kuhusu yeyote kukaribia kiongozi wake akiwa na silaha.

Alitoa mfano wa mwezi Machi mwaka jana wakati waziri mkuu wa Canada anayeondoka Justin Trudeau aliweka mkono wake kwa kifua cha Putin, walinzi wake wakataka kuchukua hatua lakini Putin akawakanya kwa ishara ya mkono.

“Viongozi wa Afrika wanafaa kutarajia heshima sawa na hiyo kutoka kwa wenzao wa mataifa ya Afrika.” aliongeza Omokri akisema kwamba kiongozi wa Afrika anapomchukulia mwenzake kwa njia hiyo naye anafaa kutarajia hatua sawa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *