Redsan kusherehekea miaka 30 katika muziki

Ataandaa tamasha ya Redsan@30 katika uwanja wa Carnivore jijini Nairobi, Agosti 29, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Swabri Mohammed maarufu kama Redsan, mwanamuziki wa Kenya wa mitindo ya reggae na ragga anaandaa tamasha ya kuadhimisha miaka 30, katika tasnia ya muziki.

Redsan amekuwa akitangaza tamasha hiyo ya Redsan@30 itakayoandaliwa Agosti 29, 2026, kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii na kulingana naye, tiketi alizotoa awali za mashabiki sugu tayari zimenunuliwa zikaisha.

Tiketi hizo zilikuwa zinauzwa shilingi elfu mbili kila moja na zimenyakuliwa na mashabiki wanaotamani kujionea mazuri ya Redsan ya miaka 30 katika uwanja wa Carnivore jijini Nairobi.

Redsan alianza kuimba akiwa na umri mdogo lakini tukio lililomzindua rasmi ni la huko huko Carnivore la mwaka 1998 la kutafuta talanta za muziki.

Alizaliwa na kulelewa mtaani Majengo jijini Nairobi, lakini asili ya wazazi wake ni Pwani na yeye ni wa kabila la Duruma, mojawapo ya makabila ya Mijikenda.

Albamu yake ya kwanza iitwayo “Seasons of the San”, ilizinduliwa mwaka 2002 akiwa chini ya usimamizi wa Ogopa Deejays. Redsan alijipatia umaarufu na kua msanii mkubwa ambaye anaandaa tamasha za kimataifa baada tu ya kuzindua albamu hiyo ya kwanza.

Red na Pioneer ndizo albamu zake za pili na tatu alizozindua miaka ya 2004 na 2006 mtawalia na kulingana na mashabiki wa mtindo wake wa muziki, zilikuwa kazi bora.

Kufikia sasa ana jumla ya albamu 6, zikiwemo Versatility aliyozindua mwaka 2009 na The Baddest ya mwaka 2018.

Mwanamuziki pekee ambaye amefichua kwamba atahudhuria tamasha hiyo ni Jose Chameleone wa asili ya Uganda, ambaye walianza naye kazi ya muziki chini ya Ogopa Deejayz.

Share This Article