Ray G aanzisha mchango wa Jose Chameleone

Joseph Mayanja au Jose Chameleone amekuwa nchini Marekani kwa miezi karibu minne kwa ajili ya matibabu.

Marion Bosire
2 Min Read
Ray G

Mwanamuziki wa Uganda Ray G ameanzisha mchango ambao kulingana naye, unalenga kupiga jeki urejeo wa mwanamuziki nguli Jose Chameleone kutoka Marekani.

Joseph Mayanja au Jose Chameleone amekuwa nchini Marekani kwa miezi karibu minne kwa ajili ya matibabu.

Ray G analenga kuchangisha shilingi bilioni moja pesa za Uganda ambazo ni sawa na milioni 35 za Kenya za kusaidia kigogo huyo wa muziki.

Chini na mpango huo wa mchango, Ray G anahimiza mashabiki wa Chameleone kote nchini Uganda watoe shilingi elfu 10 kila mmoja akipania kuafikia mashabiki laki moja.

Alielezea kwamba fedha hizo ni za kumshukuru Chameleone kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki nchini Uganda kwa miaka mingi sasa.

“Tasnia ya muziki nchini Uganda inastawi sasa kwa sababu yeye alianzisha moto huo. Anabeba bendera ya Uganda katika kila jukwaa. Anarejea nyumbani karibuni. Tumpe tulichonacho kwa upendo kwa kumchangishia bilioni moja.” aliandika Ray G kwenye mtandao wa X.

Tayari kampuni kama MTN Uganda na Airtel Uganda zimetumiwa maombi ya kutoa kodi spesheli za kutuma pesa hizo kulingana na Ray G.

Chameleone ambaye alisafirishwa hadi Marekani kwa matibabu Disemba 2024, anaonekana kupata nafuu kutokana na picha na video ambazo amekuwa akichapisha mitandaoni.

Anatarajiwa kuhudhuria na kutumbuiza kwenye tamasha la Sanyu Sanyu ambalo amekuwa akitangaza litakalofanyika Lugogo, Mei 17, 2025.

Website |  + posts
Share This Article