Jumbe za rambirambi zinazidi kutolewa na viongozi mbalimbali kufuatia kufariki kwa Rais wa Namibia Hage Geingob mapema leo Jumapili.
Aliyekuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ndiye wa hivi punde zaidi kutoa ujumbe huo akisema maneno hayawezi kuelezea pengo ambalo ameacha kiongozi huyo.
Uhuru amemtaja Geingob kuwa kiongozi aliyejitolea kutumikia watu wake na alikuwa mwenye busara sana.
“Tutazidi kukumbuka na kuthamini mchango wake mkubwa kwa ustawi na maslahi ya watu wa Namibia na Afrika kwa jumla,” alisema Uhuru kupitia taarifa.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga naye ametoa pole zake kwa familia ya Rais Geingob na watu wa Namibia.
Kulingana na Raila, bara la Afrika limepoteza kiongozi wa kweli na mtetezi wa kweli ambaye atakumbukwa kwa mchango wake wa kupigania uhuru.
Alitaja pia jukumu lake katika uundaji wa katiba ya Namibia, kitu ambacho anasema kitasalia katika nyoyo za watu wa Namibia kwa muda mrefu.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hajasazwa katika kutoa pole zake kwa familia ya Geingob na watu wa Namibia.
“Kwa niaba ya watu wa Tanzania, natuma risala zangu za pole kwa watu wa taifa la Namibia, kaimu Rais Dkt. Nangolo Mbumba, mkewe rais Geingob Monica Kalondo, familia, marafiki na wendani katika chama cha SWAPO,” alisema kiongozi huyo wa Tanzania kwenye taarifa.
Rais Geingob alifariki leo Jumapili alfajiri akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja katika jiji kuu la nchi yake, Windhoek.