Rais aliyeondolewa madarakani wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol amekamatwa.
Yoon alikamatwa leo Jumatano kutokana na jaribio lake lililoshindikana la kutangaza sheria ya kijeshi.
Hatua hiyo inatamatisha mivutano iliyodumu wiki moja kati yake na mamlaka na kumfanya kuwa Rais wa kwanza aliye madarakani kukamatwa katika historia ya nchi hiyo.
Yoon, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uasi kutokana na juhudi zake zilizodumu muda mfupi za kutangaza sheria ya kijeshi mwezi jana, alisema atashirikiana na wapelelezi ili kuepusha “umwagikaji damu”.
Akiwa mwendesha mashtaka wa zamani aliyekiongoza chama cha kihafidhina cha People Power Party (PPP) kushinda uchaguzi mwaka 2022, Yoon huenda akakabiliwa na hukumu ya kifo au akafungwa jela ikiwa atapatikana na hatia ya uasi.
Alikwepa kukamatwa kwa wiki kadhaa kwa kusalia katika makazi ya Rais akilindwa na wanachama wa Idara ya Usalama wa Rais (PSS) waliosalia waaminifu kwake.
Yoon, ambaye alikuwa ameapa “kupigana hadi mwisho”, alifanikiwa kuzuia jaribio la kwanza la kumkamata Januari 3 kutokana na mivutano iliyodumu muda mrefu kati ya walinzi wake na wapelelezi wa kupambana na ufisadi waliofanya kazi na maafisa wa polisi.
Lakini leo Jumatano, wapelelezi waliwasilisha kibali kipya kwa walinzi wa Yoon, na walilazimika kupita mabasi yaliyowekwa kuwazuia na kukata seng’enge ili kuingia kwenye makazi ya rais, kwa mujibu wa afisa mmoja wa upelelezi.