Rais Ruto apongeza RSF kwa kujitolea kumaliza mzozo Sudan

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amepongeza kundi la Rapid Support Forces, RSF kwa kujitolea kutafuta suluhisho la kudumu kwa mzozo unaoshuhudiwa nchini Sudan.

Rais Ruto alifanya mazungumzo na kiongozi wa kundi hilo la RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo katika ikulu ya Nairobi.

Kiongozi wa nchi anaamini kwamba mazungumzo ya pande mbili yanayoongozwa na mamlaka ya maendeleo kati ya serikali mbalimbali, IGAD yataafikia suluhisho la kukomesha vita nchini Sudan.

“Tunatizamia utatuzi wa mzozo huo kwa njia ya amani na kuwa na jirani thabiti,” alisema Ruto.

Kundi la RSF limekuwa likipigana na wanajeshi wa serikali nchini Sudan tangu Aprili 15, 2023 wakati Ramadhan ilikuwa ikiendelea.

Vita hivyo vilianzia katika jiji kuu Khartoum na eneo la Darfur na kufikia sasa watu wapatao elfu 10 wameuawa kwenye mzozo huo, elfu 12 wamejeruhiwa na wengine zaidi ya milioni 6 wamehama makazi yao kwa hofu ya kushambuliwa.

Raia milioni 1.5 wa Sudan wametorokea nchi nyingine kama wakimbizi kwa sababu ya vita hivyo.

Share This Article