Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev amechaguliwa tena kuongoza nchi hiyo baada ya kuzoa asilimia 87.1 ya kura zote zilizopigwa kwenye uchaguzi wa Jumapili. Haya ni kulingana na tume ya uchaguzi nchi humo.
Mirziyoyev, ambaye ameongoza nchi hiyo tangu mwaka 2016, aliandaa uchaguzi mapema baada ya kubadilisha katiba kupitia kura ya maoni na kuongeza kipindi cha uongozi wa rais kutoka miaka mitano hadi miaka saba.
Alikuwa akishindana na wanasiasa wengine watatu ambao hawana umaarufu na hivyo alitarajiwa kuibuka mshindi.
Awali, Mirziyoyev alihudumu kama waziri mkuu chini ya aliyekuwa rais Islam Karimov na akaonyesha mtindo wa uongozi wa mageuzi tangu alipoingia mamlakani huku akiahidi kujenga Uzbekistan mpya.
Alitekeleza mageuzi yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda ambayo yalipunguza ushuru, yakaondoa vikwazo vya kufanya biashara na kuwezesha wengi kusuluhisha mizozo ya urasimu kupitia maombi kwenye tovuti ta rais.
Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini humo yanasema haki za binadamu zimeheshimiwa zaidi chini ya uongozi wa Mirziyoyev. Alimaliza utumwa kwenye mashamba ya pamba na akaachilia wafungwa wa kisiasa waliokamatwa wakati wa uongozi wa Karimov.
Serikali yake hata hivyo inalaumiwa kwa kulemaza juhudi za kuafikia demokrasia.