Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametuma risala za rambirambi kwa Rais William Ruto na raia wa Kenya, kufuatia kifo cha mkuu wa vikosi vya ulinzi Jenerali Francis Ogolla, na wanajeshi wengine tisa.
“Natuma salamu za pole kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Mheshimiwa William Ruto, wananchi wote wa Kenya, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa wote waliopoteza jamaa zao katika katika ajali hiyo. Poleni sana,” aliomboleza Rais Samia.
Rais Samia aliongeza kuwa,”Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla na wanajeshi wengine tisa katika ajali ya helikopta iliyotokea leo katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet,”.
Jenerali Ogolla alifariki pamoja na wanajeshi wengine tisa Alhamisi alasiri katika ajali ya helikopta aina ya Huey, katika eneo la Sindar, kaunti ya Elgeiyo Marakwet.
Rais Ruto ametangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa, kuomboleza vifo vya wanajeshi hao waliofariki kuanzia Ijumaa Aprili 19, 2023.