Rais wa Liberia George Weah ashindwa katika uchaguzi wa Urais

Tom Mathinji, BBC and BBC
2 Min Read

Rais wa Liberia George Weah, amempigia simu mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha urais, Joseph Boakai, kumpongeza kwa ushindi wake

Katika hotuba kwa taifa, Weah alisema “watu wa Liberia wamezungumza na tumesikia sauti yao”.

Mgombea wa upinzani anaongoza kwa kura 28,000 huku takriban kura zote zikiwa zimehesabiwa.

Nyota huyo wa zamani wa kandanda, amekuwa madarakani tangu 2018 na ataondoka uongozini mnamo mwezi Januari.

Aliingia katika kiti cha urais akiwa na shauku, hasa kutoka kwa wapiga kura vijana, baada ya kushinda uchaguzi huo dhidi ya Boakai kwa tofauti kubwa.

Lakini dhana kwamba ameshindwa kukabiliana na ufisadi, kupanda kwa gharama ya maisha na kuendelea kwa matatizo ya kiuchumi kuliharibu sifa yake.

Weah alieleza kwa hekima kuwa ameshindwa, akianza hotuba yake ya dakika tano kwa kusema “anaheshimu sana mchakato wa kidemokrasia ambao umelifafanua taifa letu”, akiongeza kuwa alizungumza na Boakai ambaye alimwita “rais mteule”.

Hapo awali tume ya uchaguzi ilitangaza kuwa Boakai, mkongwe wa kisiasa mwenye umri wa miaka 78 alikuwa na asilimia 50.89 ya kura, huku Rais Weah akiwa na 49.11%.

Rais alirejelea ukaribu wa kinyang’anyiro hicho akisema “unafichua mgawanyiko mkubwa ndani ya nchi yetu” na kutoa wito kwa Waliberia “kushirikiana kutafuta muafaka… umoja ni muhimu kwa mama Liberia”.

Kipindi kirefu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo takriban watu 250,000 walifariki dunia kilimalizika miaka 20 iliyopita

Website |  + posts
Share This Article