Bunge la Korea Kusini limembandua mamlakani Rais Yoon Suk Yeol,siku ya Jumamosi kufuatia hatua yake ya kuanzisha sheria za kijeshi kwa raia.
Bunge limefanikiwa kumng’atua Yoon leo baada ya jaribio la kwanza kugonga mwamba wiki jana, wakati wabunge wa upande wa serikali walikataa kushiriki kwa kura hiyo iliyoitishwa na wabunge 199 wa upinzani.
Licha ya kutimuliwa Rais Yoon ataendelea kusalia mamlakani na kuendelea kupewa ulinzi pamoja na marupurupu yake.
Hata hivyo kulingana na katiba ya nchi hiyo Yoon, hana uwezo wa kuidhinisha sheria yoyote,kusaini mikataba ya kimataifa,kuteua mabalozi na mawaziri na pia uhuru wa kutuma vikosi vya jeshi katika vita.
Endapo mahakama itathibitisha kutimuliwa kwake Yoon ndani ya miezi sita ijayo atapoteza mafao na marupurupu yake yote na kuondoka afisini.