Rais wa Hungary Katalin Novak alijiuzulu Jumamosi Februari 10, 2024 baada ya shinikizo kuzidi kutokana na hatua yake ya kutoa msamaha kwa mtu aliyehukumiwa kwa kosa la kusaidia mwingine kufunika hatia ya ubakaji katika makazi ya watoto yatima.
Novak, amejiuzulu yapata wiki moja tangu msamaha huo wa Rais ufahamike na umma na kusababisha lalama pamoja na shinikizo za kujiuzulu.
Aliyekuwa waziri wa haki na sheria Judit Varga pia alitakiwa kujiuzulu na alijiuzulu kutoka wadhifa wa mbunge Jumamosi.
Suala hili limekuwa kikwazo kikubwa kwa waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban ambaye ni rafiki wa karibu wa Katalin Novak.
Orban, amekuwa mamlakani tangu mwaka 2010 na sasa anajiandaa kwa kinyang’anyiro kingine kwenye uchaguzi wakati nchi hiyo inapona kutokana na mfumko wa bei za bidhaa.
Katika muda wa miaka mingi, Orban amekuwa akitetea kulindwa kwa watoto kutokana na watu aliowataja kuwa wanaharakati wa ushoga ambao walikuwa wakirandaranda kwenye shule za nchi hiyo.
Novak ambaye alitangaza kujiuzulu kwake kupitia runinga aliomba msamaha akikiri kwamba alifanya makosa na kwamba hiyo ilikuwa hotuba yake ya mwisho kama Rais.
Alikatiza ziara yake huko Qatar ghafla na kurejea jijini Budapest Jumamosi.
Alielezea kwenye hotuba hiyo jinsi alitoa msamaha kwa mfungwa huyo Aprili mwaka jana akiwa na imani kwamba hakuhusika katika kudhulumu watoto aliokuwa akiwatunza.
Waziri mkuu katika hatua ya kurekebisha kosa hilo na kuzuia kutendeka kwake siku za usoni alitumia bunge Alhamisi kurekebisha sheria ambapo alimpokonya Rais uwezo wa kutoa msamaha kwa watu waliohukumiwa kwa makosa yanayohusu watoto.