Rais wa Georgia Salome Zourabichvili amesema hataondoka madarakani muhula wake utakapofikia kikomo, kwa sababu ya kile anachokitaja kuwa bunge haramu.
Anataka uchaguzi urudiwe huku waziri mkuu akionya kuhusu uwezekano wa mapinduzi wakati maandamano yanayopendelea umoja wa ulaya yanaendelea.
Raia wengi wa Georgia waliandamana jana Jumamosi kwa siku ya tatu mfululizo baada ya waziri mkuu Irakli Kobakhidze kutangaza kwamba serikali itasimamisha mazungumzo kuhusu kujiunga na umoja wa Ulaya.
Lengo la kujiunga na umoja huo wenye wanachama 27, sasa limekitwa kwenye katiba ya Georgia, lakini waziri mkuu ambaye amekuwa akoboresha uhusiano wake na Russia alisimamisha mazungumzo hayo kwa miaka minne.
Alilaumu Brussels kwa kile alichokitaja kuwa usaliti.
Katika hotuba yake ya Jumamosi, Rais Zourabichvili, alisema kwamba bunge halina haki ya kuchagua atakayechukua mahala pake muhula wake unapoisha Disemba na ataendelea kushikilia uongozi.
Rais ambaye mamlaka yake ni ya kitaratibu tu anashikilia kwamba uchaguzi wa Geogia wa Oktoba 26 ambao chama cha Georgian Dream kilishinda kwa asilimia 54 ulijawa ulaghai na hivyo wote waliochaguliwa ni haramu.
Mapema mwezi Novemba, tume ya uchaguzi ya Georgia ilitambua chama tawala kama mshindi lakini wadadisi na wanasiasa katika Umoja wa Ulaya na Marekani pia wamependekeza uchunguzi kuhusu madai ya ulaghai katika uchaguzi huo.