Rais Tshisekedi atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini DRC

Marion Bosire
2 Min Read

Rais Félix Tshisekedi ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Urais katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, matokeo ambayo wagombea kadhaa wa upinzani wamepinga wakitaka uchaguzi urudiwe.

Rais Tshisekedi alishinda kwa asilimia 73 ya kura zilizopigwa huku mshindani wake wa karibu mwanabiashara Moise Katumbi akipata asilimia 18 ya kura zote zilizopigwa.

Kulingana na takwimu wapiga kura waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 40, sawa na watu milioni 18.

Uchaguzi huo wa Disemba 20, 2023 ulikumbwa na matatizo mengi ya kimpangilio ambapo vituo fulani viliongezewa muda wa kupiga kura kwa siku moja katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Vituo vingi vya kupigia kura havikufunguliwa kwa wakati na mitambo mingi ya kupigia kura ilikosa kufanya kazi siku ya kwanza ya kupiga kura.

Wengi walisubiri kwa muda mrefu kabla ya kupiga kura huku wengine wengi wakikosa subira na kurejea nyumbani bila kupiga kura.

Upinzani unahisi kwamba matatizo hayo yalipangwa kama njama ya kuiba kura na kumpendelea Rais Tshisekedi.

Wanajeshi wametumwa kwenye sehemu kadhaa mjini Kinshasa kuzuia ghasia huku wafuasi wa Tshisekedi wakisherehekea barabarani.

Wanaopinga matokeo hayo wana muda wa siku mbili kuwasilisha malalamishi yao katika mahakama ya kikatiba.

Mahakama hiyo itatumia muda wa siku 7 kutatua kesi hizo huku Tshisekedi akitarajiwa kuapishwa mwisho wa mwezi huu wa Januari mwaka 2024.

Share This Article