Rais Samia kuongoza hafla ya kuaga mwili wa Dkt. Ndugulile leo

Hafla hiyo inaandaliwa katika uwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na tayari mwili huo umefikishwa huko.

Marion Bosire
1 Min Read
Rais Samia Hassan kwenye mazishi ya Edward Lowassa awali

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu anatarajiwa kuongoza hafla ya kuaga mwili wa Dkt. Faustine Ndugulile, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, WHO kanda ya Afrika.

Hafla hiyo inaandaliwa katika uwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam na tayari mwili huo umefikishwa huko.

Dkt. Ndugulile alifariki Novemba 27, 2024, akiwa na umri wa miaka 55, miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo wa WHO.

Alistahili kuchukua mahali pa Dkt. Matshidiso Moeti wa Botswana ambaye amehudumu kwa miaka mitano, kuanzia mwezi Februari mwakani.

Ndugulile ambaye alikuwa daktari na mbunge wa eneo la Kigamboni alifariki akipokea matibabu nchini India.

Alipata umaarufu wakati wa uongozi wa Hayati Rais John Magufuli wakati wa janga la virusi vya korona mwaka 2020 wakati huo akihudumu kama Waziri Msaidizi wa Masuala ya Afya.

Baada ya hafla ya leo ya kitaifa, mwili wa Dkt. Ndugulile utapelekwa nyumbani kwake huko Kigamboni na kesho utawekwa katika uwanja wa Machava kwa ajili ya kuagwa na wakazi.

Wakazi wakimaliza kuuaga, utapelekwa katika kanisa katoliki la Virgin Mary Consolata kwa ajili ya misa na hatimaye mazishi katika makaburi ya Mwongozo kati ya saa tisa unusu na saa kumi na moja unusu jioni.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *