Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameteua maafisa ambao watajazanyadhifa tano, kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari.
Taarifa hiyo ambayo imetiwa saini na mkurugenzi wa mawasiliano katika Ikulu ya Tanzania Sharifa B. Nyanga, inaorodhesha uteuzi wa mhandisi Ramadhani Masoud Lwamo kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.
Lwamo ambaye utaalamu wake ni katika nyanja ya uchimbaji madini amekuwa akihudumu kama kaimu katika wadhifa huo.
Dkt. Aggrey Kalimwage Mlimuka naye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani (FCC) kwa kipindi cha pili huku Prof. Othman Chande Othman akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kipindi cha pili.
Wengine walioteuliwa na Rais Samia ni Dkt. Florens Martin Turuka ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kipindi cha pili na Prof. Valerian Cosmas Silayo ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini
(CAMARTEC) kwa kipindi cha pili.