Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amehimiza wasanii nchini Tanzania kukoma kuzozana na badala yake kushirikiana na kutia bidii katika kazi zao.
Akizungumza katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam jana usiku wakati wa uzinduzi wa Albamu ya Harmonize, kiongozi huyo alisema kwamba anawajali sana wasanii na atahakikisha maslahi yao yametiliwa maanani na serikali.
Rais Samia alisema kwamba wanaposhirikiana kama wasanii wanakua kwa pamoja na wanapokua kwa wingi basi Tanzania inakua.
Harmonize alitengeneza albamu ya nyimbo kumi ambazo zote zinamhusu Rais Samia Suluhu Hassan na akaipa jina la “Muziki wa Mama” ndiposa akamwalika kuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo.
Kati ya nyimbo hizo kumi, Rais Samia alisema aliguswa zaidi na nyimbo mbili, moja ni “Never Give Up” ambayo inahimiza watu kutokata tamaa na nyingine inayosema kwamba mwanamke ni mtu na nusu.
Alimpongeza Harmonize kwa kujikaza hadi akafika aliko sasa kama msanii akisema kila mmoja ana mapito yake na ni lazima kuwe na ukuaji kupitia kwa kutokufa moyo.
“Nilikuwa namsikiliza Harmonize alivyokuwa anasema hadithi zake alivyo-hustle yanayomkuta, ni safari ambayo wengi wetu tumepita, ndio maana nikasema kuna ukuaji kutoka alipotoka mpaka alipo, katikati hapa kuna mapambanao yanayowapata vijana ikiwemo lile alilotuambia la mahusiano mpaka anatendwa ndio anatia adabu anasema sasa nabaki na huyu.” alisema Rais Samia huku akitaja wanamuziki Rayvanny, Ommy Dimpoz na Diamond Platnumz akisema wote pia waliyapitia.
Harmonize ameandikisha historia ya kuwa mwanamuziki wa kwanza wa Bongo Flava kuwa na Rais Samia kwenye hafla yake.