Ruto: Ujenzi wa nyumba za gharama nafuu hautasitishwa

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto ameelezea kujitolea kwake kufanikisha mpango wa serikali wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini, akisema kwamba hauwezi kusitishwa.

Rais alikariri kuwa ana nia kubwa ya kuboresha taifa hili.

Akiongea jana Jumanne alipoongoza hafla ya kuzindua mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo bunge ya Soy na Kapseret katika kaunti ya Uasin Gishu, Rais Ruto alisikitika kuwa taifa hili limejikokota katika kuafikia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Alisema kuwa mataifa kadhaa yalianzisha mipango kama hiyo miongo kadhaa iliyopita. Kiongozi wa taifa alikariri kwamba utekelezaji wa mpango huo utahakikisha Wakenya wamepata makazi bora na ya gharama nafuu.

Rais aliahidi kukabiliana na wale wanaotumia mfumo wa mahakama kulemaza sera na mipango yake.

Alisema watu wanaowasilisha kesi mahakamani kusimamisha mipango yake hawajui mahangaiko wanayowasababishia vijana walioelimika, walio na ujuzi na ambao hawana ajira.

Baadaye, Rais alihudhuria hafla ya kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa la Eldoret 64 mjini Eldoret.

Share This Article